Sarufi za Kiswahili : sehemy ya 3


9. VIHISISHI / VIINGIZI
            Ni maneno ambayo hudokeza hisia za moyoni mwa mzungumzaji baada ya kuwa katika hali ya furaha, huzuni, majonzi, maumivu, kushangaa, majuto n.k. Mara tunapotumia viingizi katika tungo huathiri tungo hiyo kuifanya kuwa na mshangao, hivyo tunaongeza alama ya mshangao mbele ya tungo hiyo. Kwa kuzingatia hisia tunaweza kuwa na aina ya viingizi zifuatazo:-
·         Viingizi vya huzuni – pole! Jamani! Maskini! N.k
·         Viingizi vya mshangao – waow! Lahaula! Eboo! Haiii! Ati!
·         Viingizi vya kuitika – abee! Lamaa! Naam!
·         Viingizi vya kutakia heri – Inshallah!
·         Viingizi vya kiapo – Wallah! Haki ya nani! Kweli kabisa!
 ZOEZI
1.      Tofautisha majina dhahania naya kipekee.
2.      Fafanua matumizi matano ya vitenzi vishirikishi kwa mifano bayana.
3.      Ainisha maneno katika sentensi zifuatazo:-
a.       Mtoto mzuri ameondoka.
b.      Yusuph na Ndonje hawaelewani.
c.       Kwenye kikapu kuna mboga.
d.      Loo! Huna aibu kumuita.
e.       Atakayekuja awe amejiandaa kujibu maswali.
f.       Nimesoma kitabu lakini sijagundua kinahusu nini.
g.      Mkaribishe, aingie.
h.      Nataka nikija nikute tayari.
i.        Ustaarabu umenishinda.
j.        Mwalimu alisema, tuonane kesho.
4.      Tunga sentensi ukionmesha matumizi matano ya kihusishi ‘kwa’.
5.      Kwa kutumia mifano eleza tofauti ya viunganishi na vihusishi.
6.      Eleza kwa mifano bayana aina tatu za vitenzi.
7.      Onesha matumizi matano ya vielezi katika sentensi.
8.      Kivumishi ni nini? Onesha matumizi matano ya vihusishi vya nomino.
9.      Tunga sentensi sita kwa kila aina ya kiunganishi.
10.  Tumia viingizi vifuatavyo kutunga sentensi sahihi:
a.       Taibu
b.      La hasha
c.       Salale
d.      Mashallah
e.       Ebo
1.      SARUFI MUUNDO
Sarufi muundo hujihusisha na kushughulikia mpangilio na mfuatano wa maneno katika tungo ili yaweze kujitosheleza kimaana. Katika sarufi muundo tunaangalia mijengo ya tungo za kiswahiali.

                                    TUNGO
            Tungo ni huwa ni matokeo ya kuviweka pamoja vipashio sahili vya lugha ili kujengana hata kipashio kikubwa kabisa cha lugha. Tungo ina asili yake katika mzizi ‘Tunga’ ukiwa na maana ya kuibua kitu kipya kabisa au kushikamanisha vitu pamoja ili kupata ‘utungo’.
            Tungo hujidhihirisha katika viwango vine ambavyo hutupatia vipashio vya tungo:-
Ø  Kiwango cha neno ambacho hujengwa na mofimu
Ø  Kiwango cha kirai ambacho hujengwa na neno
Ø  Kiwango cha kishazi ambacho hujengwa na kirai
Ø  Kiwango cha sentensi ambacho hujengwa na kirai au kishazi

1.      NENO
Ni silabi au mkusanyiko wa silabi zinazotamkwa na kuandikwa na kuleta maana katika lugha husika. Neno huundwa na mofimu. Ikiwa ni mofimu huru neno huwa neno huru lakini neno likiundwa na mofimu tegemezi neno huwa changamano. Zipo aina nane za maneno katika lugha ya Kiswahili ambazo ni:-
                                i.            Nomino
                              ii.            Kivumishi
                            iii.            Kiwakilishi
                            iv.            Kitenzi
                              v.            Kielezi
                            vi.            Kiunganishi
                          vii.            Kihisishi na
                        viii.            Kihusishi. (rejelea aina za maneno kwa ufafanuzi zaidi)1.      KIRAI
Ni kipashio cha lugha ambacho huwa na muundo wa neno moja au zaidi lakini huwa hakina muundo wa kiima na kiarifu. Muundo wa kirai huwa ni wa neno moja au zaidi ambayo huwa pamoja katika mpangilio maalumu wenye kuzingatia uhusiano wa maneno hayo na neno kuu ambalo ndio huwa linabeba aina ya kundi hilo la maneno.
            AINA ZA VIRAI
A.    Kirai nomino (KN)
Hili ni kundi la maneno ambalo hutawaliwa na nomino. Kirai nomino huundwa na maneno yafuatayo:-
o   Nomino pekee. Mfano; Asha anapika, Nyangoye anaimba, Nyegera anacheza (N)
o   Nomino mbili au zaidi zinazounganishwa. Mfano; Mhindi na Sagatiwanacheza. (N+U+N)
o   Nomino na kivumishi. Mfano; Mtoto mnene amekuja, Mzee mfupiameondoka. (N+V)
o   Kiwakilishi pekee. Mfano; Yule ameondoka, Wewe umenena, Walewaliokuja. (W)
o   Kiwakilishi na kivumishi. Mfano; Yule mvivu amerudi, Wewe mlemavunjoo. (W+V)
o   Nomino na kitenzi jina. Mfano; Mchezo wa kusisimuaWimbo wa kupendeza. (N+Ktj)
o   Nomino na kishazi tegemezi kivumishi. Mfano; Mjukuu aliyepotea, Mheshimiwa aliyeondoka. (N+βV)
B.     Kirai kivumishi (KV)
Hiki ni kirai ambacho muundo wake umejikita katika kivumishi na maneno yanayohusiana na kivumishi katika tungo tungo hiyo. Virai hivi kwa kawaida hujibainisha zaidi kimuundo kama sehemu ya virai nomino. Virai hivi huundwa na:-
o   Kivumishi na Kirai nomino. Mfano; Mwenye mali nyingiWenye watoto wengi.
o   Kivumishi na kielezi. Mfano; Mzuri sana, Mweupe pee!,Mweusi tii!, Mbaya sana.
o   Kivumishi na kirai kitenzi. Mfano; Mwenye kupiga gitaaMwenye kupenda sana.
o   Kivumishi na kirai kiunganishi. Mfano; Nzuri ya kupendezaMpungufu wa akili.
C.    Kirai kitenzi (KT)
Ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi, au katika uhusiano wa kitenzi na neno au mafungu ya mengine ya maneno. Hii ina maana kwamba, neno kuu katika kirai hiki ni kitenzi. Kirai kitenzi kimeundwa na vipashio vifuatavyo:-

o   Kitenzi pekee. Mfano; amekujaamekulaameoga. (T)
o   Kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu. Mfano; Alikua anacheza(Ts+T), Alikua anaweza kuimba. (Ts+Ts+T)
o   Kitenzi kishirikishi na shamirisho. Mfano; Ni mtanashatiNdiye mwiziSio mwelewa. (t+sh)
o   Kitenzi, jina na kielezi. Mfano; Nimepika uji asubuhi
D.    Kirai kielezi
Tofauti na aina nyingine ya virai, miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi ) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo. Zaidi kirai kielezi huelezea namna, wakati, mahali na kinachofanya tendo hilo litendeke. Mfano; Mara nyingi, Sana sana, Polepole, Jana asubuhi, Kesho mchana, n.k.
E.     Kirai kihusishi
Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya vihusishikwa, na, katika,au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno menginekirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kihusishi. Virai vihusishi japokuwa muundo wake hufanana ila hutofautiana kimaana, zipo maana tatuambazo ni:-
a)      Pahala – kwa baba, katika kabati, kwenye lindo
b)      Utumizi – Kwa kisu, Kwa mkono
c)      Uhusika – Na Mjomba, Na Bibi.
Vilvile kirai kihusishi hutumiwa kutekeleza majukumu yafuatayo katika sentensi:-
ü  Kama kivumishi. Mfano; Penseli ya mjomba, Mkoba wa mama, Koti la babu
ü  Kama kielezi. Mfano; Tulisikiliza kwa makini, Tuliimba kwa shangwe, Tulisoma kwa juhudi
ü  Kama kiwakilishi. Mfano; La mjomba limetupwa, Ya shangazi imeuzwa, Wa nne ameondoka2.      KISHAZI
Ni aina ya tungo ambayo huwa na kitenzi ndani yake, kitenzi hicho kinaweza kikawa kinakamilisha maana au kisiwe kinajikamilisha kimaana. Kitenzi ambacho huwa kinakamilisha maana huwa ni kitenzi kikuu (T), na kile kisichokuwa kinatoa taarifa kamili huwa ni kitenzi kisaidizi (TS). Kwa mujibu huo tunapata aina mbili za kishazi yaani kishazi huru na kishazi tegemezi.
A.    Kishazi huru (K/Hr)
Aina hii ya kishazi huwa na tabia ya kutoa taarifa ambayo huwa ni kamili katika tungo, hubeba kitenzi kikuu au kishirikishi ndani yake. Kishazi hiki huwa hakihitaji maelezo ya ziada ili kukamilisha maana au taarifa kusudiwa na pia huweza kujitegemea kama sentensi kamili na huwa na muundo wa kiima na kiarifu.
Mfano; Mtoto / anacheza mpira
                  K                     A
            Mwanafunzi / anasoma kitabu
                  K                     A
            Mwanaume / anakufahamu
                  K                     A
           Mwanafunzi /. ni mpole
                  K                     A
B. Kishazi tegemezi (K/ Tg)
Aina hii ya kishazi huwa haitoi taarifa iliyokamili badala yake hutegemea kishazi huru ili kukamilisha taarifa iliyokusudiwa na msemaji. Kishazi hiki hutawaliwa na kitenzi kisaidizi. Kishazi tegemezi kwa upekee wake hakiwezi kutoa taarifa iliyokusudiwa. Vishazi tegemezi hushuka hadhi na kuwa na hadhi ya kikundi cha maneno (kirai).
Mfano;      Mtoto unayemjua
                  Mwanafunzi anayesoma
                  Mahali alipoingia
                  Mama alipomchapa
                  Kaka aliporudi
Vishazi hivyo hapo juu havitoi taarifa iliyokamili ila tunapoviweka pamoja na vishazi huru taarifa iliyokusudiwa hukamilika. Tazama hapa chini:-
Mfano;       Mtoto unayemjua ameondoka
                  Mwanafunzi anayesoma atafaulu
                  Mahali alipoingia ni pachafu
                  Mama alipomchapa aliondoka
                  Kaka aliporudi alinifurahisha
Sifa za kishazi tegemezi
                    i.            Hakikamilishi taarifa pasipokuwepo na kishazi huru
Mfano;       Mtoto anayecheza mpira ameumia
                  Mvulana aliyefaulu mtihani amefurahi
                  Mama alipomkaribisha aliingia ndani
                  ii.            Kinaweza kuondolewa katika tungo bila kuathiri taarifa kusudiwa.
Mfano;      mtoto aliyeugua amepona
                  Mtoto amepona
                  Mama uliyemsalimia pale ameondoka jana.
                  Mama ameondoka jana
                iii.            Hutambulishwa na vitambulishi vya urejeshi vinavyopachikwa katika vitenzi.
Mfano; Anayesoma, Alichookota, Uliokatika, Iliyoibiwa, Alipoingia n.k.
                iv.            Vilevile kashazi tegemezi hutambulishwa na viunganishi tegemezi kwamba, ili, ili kwamba, kwa sababu, mzizi wa amba na kiambishi cha masharti.
Mfano;       Mama alisema kwamba motto ameumia
                  Mvulana ambaye ni kaka yangu amerejea nyumbani
                  Akijua atanichapa
            Vishazi tegemezi vipo vya aina mbili kutokana na majukumu yake kimuundo
A.    Kishazi tegemezi kivumishi (bV)
Kishazi tegemezi kivumishi hufanya kazi ya kuvumisha nomino katika tungo.
      Mfano;            Baba anayenijali
                              Mbwa aliyepotea
                              Mwanafunzi aliyefariki
                              Uliyemuona pale
                              Aliyempenda sana

B.     Kishazi tegemezi kielezi (bE)
 Kishazi hiki hufanya kazi ya kueleza tendo katika tungo na hujitokeza kueleza dhima tofauti tofauti kama ifuatavyo:-
ü  Kueleza mahali tendo linapofanyika. Mfano; Alipoingia (mahali dhahiri), Alimochungulia (ndani ya kitu Fulani), Alikoelekea (mahali pasipo dhahiri)
ü  Kueleza wakati wa tendo. Mfano; Tulipotoka, Alipomchapa, Walipomsema n.k.
ü  Kueleza masharti katika tendo. Mfano; Akirudi, Angekuja, Angelimpiga, Angalijua n.k.
ü  Kueleza namna tendo linavyofanyika. Mfano; Alivyoimba, Walivyopendeza, Tulivyomsifu.
ü  Kueleza kasoro katika kukamilisha tendo. Mfano; Ingawaamesoma, Licha ya kufaulu, Japokua amependekezwa.
ü  Kueleza sababu ya kufanyika kwa tendo. Mfano; Kwa sababualipendeza, Kwa kuwa hujafaulu, Kwa vile umenisomesha.
                             
3.      SENTENSI
Sentensi ni fungu la maneno ambalo huwa na mhusika wa tendo na tendo lenyewe. Sentensi hujengwa na sehemu kuu mbili yaani kiima na kiarifu. Kiima hutawaliwa na mhusika wa tendo yaani nomino hivyo hubeba kirai nomino na upande wa Kiarifu hutawaliwa na taarifa ya tendo hivyo hubeba kirai kitenzi. Sentensi ndio kipashio cha juu kabisa katika darajia ya vipashio vya lugha.
Sehemu za Sentensi.
v  Kiima hukaliwa na kundi nomino ambayo huwa ni mtenda au mtendwa wa jambo linaloelezewa katika sentensi. Hiki hukaa upande wa kushoto mwa kitenzi au mwanzo ni mwa sentensi. Mfano; Mtoto amesoma, Mvulanaanapendwa.
Vipashio vya kiima.
o   Nomino pekee. Mfano; Babu amerudi.
o   Nomino  na Nomino. Mfano; Kaka na Dada wameondoka.
o   Nomino na kivumishi. Mfano; Mtoto mzuri amekojoa.
o   Kiwakilishi pekee. Mfano; Yule amevunjika mguu.
Kiwakilishi na Kivumishi. Mfano; Wewe mpole njoo hapa.
o   Kivumishi na Kiwakilishi. Mfano; Mjinga Yule ameondoka.
o   Kitenzi jina. Mfano; Kulima kunafaida nyingi.
o   Nomino na Kishazi tegemezi kivumishi. Mfano; Mtoto aliyeokolewaamerudishwa kwao.
v  Kiarifu hukaliwa na na maneno yanayoarifu tendo linavyofanyika, litakavyofanywa, lilivyofanywa. Hii ndiyo sehemu inayokuwa na umuhimu zaidi katika sentensi maana ndiyo inayotoa taarifa ya sentensi. Huweza kusimama pekee bila kiima maana wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima yaani viambishi vya nafsi.
Vipashio vya kiarifu
o   Kitenzi kikuu pekee. Mfano; Amekuja.
o   Kitenzi kisaidizi pamoja na kitenzi kikuu. Mfano; Mtoto alikua anacheza.
o   Kitenzi kishirikishi na Shamirisho. Mfano;  Asha ni mpole
o   Kitenzi kikuu na shamirisho. Mfano; Ninasoma kitabu.
o   Kitenzi kikuu na chagizo. Mfano; Anakwenda polepole.
o   Kitenzi kikuu, shamirisho na chagizo. Mfano; Anaendesha gari kwa kasi.
AINA ZA SENTENSI
1.      Sentensi sahili.
Sentensi sahili ni sentensi ambayo muundo wake ni rahisi. Huwa na muundo wa kishazi huru kimoja. Hivyo hubeba kitenzi kikuu kimoja. Kitenzi hicho kinaweza kuambatana na kitenzi kisaidizi ambacho huwa hakina kiambishi cha utegemezi. Sentensi sahili huwa haifungamani na sentensi nyingine, pia kiima chake huwa kimetajwa wazi na huundwa na kitenzi kikuu kimoja au kitenzi kishirikishi au kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu.
Muundo wa sentensi sahili
i.        Muundo wa kitenzi kikuu peke yake. Mfano;  Anakula, Anaimba, Wanacheza.
ii.      Muundo wa kitenzi kisaidizi na kitenzi kikuu.                                                                             Mfano;          Alikwenda kuchunga.                                                                                                             Huwa anakula.                                                                                                                             Alikuwa amekwenda kulinda.
iii.    Muundo wa kirai nomino na kirai kitenzi.                                                                                    Mfano; Juma ameondoka.                                                                                                             Mwajuma amelalamika sana.                                                                                                 Baba yangu amesafiri jana jioni.                                                                                              Mtoto mweupe mzuri amenibadilishia siku yangu.
iv.    Muundo wa virai vitenzi visaidizi.                                                                                                Mfano; Yusuph ni Mwalimu.                                                                                                                    Dani yumo darasani.                                                                                                                Nyegera ana gari zuri.
2.      Sentensi Changamano
Sentensi changamano huwa na muundo wa kishazi tegemezi na kishazi huru. Kishazi tegemezi huwa na hadhi ya kirai kivumishi au kirai kielezi. Huwa hakijikamilishi kimaana hivyo hutegemea kishazi huru ili kukamilisha maana. Hivyo sentensi changamano huchanganya kishazi tegemezi na kishazi huru pammoja.
Muundo wa sentensi changamano.  
i.                    Muundo wenye kishazi tegemezi kivumishi. (βV)
Mfano; Mbwa aliyepigwa jiwe ameumia vibaya.
             Kijana aliyeanguka chini ameumia.
             Mti uliokatwa umeota tena.
ii.                  Muundo wa kishazi tegemezi kielezi. (βE)
Mfano; Kijana alianguka aliposukumwa.
             Babu alifariki alipofikishwa hospitali.
             Binti alifaulu alipokazana kusoma.
3.      Sentensi shurutia
Sentensi shurutia ni aina ya sentensi ambayo ina muundo wa ngeli za masharti. Sentensi changamano huwa na vishazi tegemezi viwili. Viambishi hivyo vya ngeli ni; -ki-, -nge-, -ngali-, na –ngeli- ambavyo hujitokeza katika kitenzi na hujirudia katika vitenzi vyote viwili, havibadilishwi.
Mfano;      Akirudi, atanikuta.
                  Angeondoka, angefika mapema.
                  Angalinisalimu, ningalimwambia yote.
                  Wangeliambia, ningeliondoka.


4.      Sentensi ambatano
Sentensi ambatano huundwa na sentensi mbili au zaidi ambazo huunganishwa na kiunganishi. Sentensi ambatano huwa na miundo ifuatayo:-
i.                    Muundo wa sentensi sahili mbili au zaidi.
Mfano; Mheshimiwa ameruri lakini mzigo haukununuliwa.
            Bunge la katiba limeanza ila sina uhakika kama tutafanikiwa.
            Mtoto amerejea na wazazi wake wamefurahi.
            Yusuph amefanikiwa bila shaka atakuwa na furaha.
ii.                  Muundo wa sentensi sahili na changamano.
Mfano; Mbuzi amenunuliwa na aliyemnunua ni Baba.
            Mtoro ataadhibiwa pia atajulishwa atakapokosea.
            Baba mzazi analima ila shamba analolima si lake.
iii.                Muundo wa sentensi changamano pekee.
Mfano; Mtoto aliyekuja ameondoka na aliyemleta ameshafika kwake.
            Kijana alikasirika alipomuona ila aliyemuona sio mhusika.
            Alifurahi alipofika japokuwa alipoingia hapakumpendeza.
iv.                Muundo wa virai vitenzi visivyo na kiunganishi.
Mfano; Aambiwe, asirudie.
            Arekebishwe, asikosee.
            Mwache, aende.
            Mwombe, aondoke.
Maneno haya huwa na dhana ya kueleza nia ya kufanya jambo Fulani na huwa havibebi viambishi vya njeo pia vikitengwa huwa sentensi zinazojitegemea.
v.                  Muundo wa sentensi shurutia.
Mfano; Akija nitafurahi ila asipokuja nitahuzunika.
            Angelibakia ningelifurahi lakini angelikubali kulala ningelifurahi zaidi.

ZOEZI
1.      Fafanua dhana ya Tungo kisha taja vipashio vinavojenga tungo.
2.      Eleza tofauti ya kirai na kishazi.
3.      Kirai ni kundi la maneno. Thibitisha kwa aina zake huku ukitolea mifano toshelevu.
4.      Kwa mifano eleza maana ya:-
a.       Kishazi
b.      Kishazi huru
c.       Kishazi tegemezi
5.      Thibitisha kuwa kishazi tegemezi hufafanua nomino na kitenzi.
6.      Ainisha vishazi katika tungo zifuatazo:-
a.       Mtoto mwerevevu ameondoka.
b.      Kabla sijamfahamu nilimsumbua sana.
c.       Katika kikapu kilichojaa niliweka nguo chafu.
d.      Asiyestahili amesifiwa.
e.       Bibi aliyeshikwa uchawi ni jirani yetu.
f.       Mama alikua anapika chakula wakati wgeni walipofika.
g.      Akimaliza kusoma atatupeleka disko.
h.      Angelijua, angeliondoka mapema.
i.        Waliingia msikitini walipotaka kuswali.
j.        Vkombe visivyotakatika visitumike.
7.      Thibitisha kuwa kila sentensi ni kishazi ila si kila kishazi ni sentensi.
8.      Fafanua aina nne za sentensi kwa mifano dhahiri.
9.      Eleza kauli kuwa sentensi ambatano ni sentensi pacha zinazofanana au kutofanana.
10.  Bainisha uvumishaji na uelezi wa sentensi changamano kwa mifano.


  COMMENT BOX / SANDUKU LA MAONI