Sarufi ya kiswahili : sehemu ya 1


      SARUFI
Sarufi nimfumo na kanuni za lugha zinazomwezesha mtumiaji wa lugha kuitumia lugha husika kwa usahihi. Mfumo huo humwezesha mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na kikomo ambazo hukubalika na wazawa wa lugha wanaoifahamu lugha hiyo barabara.  Hivyo ni dhahiri kwamba kila lugha ya mwanadamu huwa na mpangilio na sheria zinazoilinda ili kuifanya kuwa toshelevu na sanifu, na uzingatiwaji wa kanuni na taratibu hizo kwa mtumiaji humfanya na kumtambulisha kama mmilisi wa lugha hiyo.
Sheria za lugha zimegawanyika katika makundi manne yanayojulikana kama matawi ya Sarufi ambayo ni pamoja na; matamshi, maumbo, muundo na maana.

1.      SARUFI MATAMSHI
Sarufi matamshi ni tawi la sarufi ambalo limejikita katika kuchunguza sauti na matamshiyanayotumika katika lugha Fulani na kulinda matumizi sahihi ya matamshi hayo baina ya watumiaji wa lugha hiyo. Lugha ya Kiswahili kama zilivyokuwa lugha zote duniani ina matamshi ya aina mbili; Irabu na konsonanti.
A.    Irabu
Irabu ni aina ya vitamkwa ambavyo hutolewa pasi na kuwepo kizuizichochote katika mkondo hewa utokao mapafuni ukipitia katika chemba ya kinywana chemba ya pua kwenda nje. Lugha ya Kiswahili inazo Irabu tano ambazo ni; /a/, /e/, /i/, /o/, na /u/.
B.     Konsonanti
Konsonanti ni aina ya sauti ambazo hutamkwa kwa kuzuia mkondo hewa kutoka mapafuni, ukipitia chemba ya kinywa na chemba ya pua kwenda nje. Katika lugha ya Kiswahili zipo jumla ya konsonanti zifuatazo; /b/, /ch/, /d/, /dh/, /f/, /g/, /gh/, /h/, /j/, /k/, /l/, /m/, /n/, /ny/, /ng’/, /p/, /r/, /s/, /sh/, /t/, /th/, /v/, /w/, /y/ na /z/.2.      SARUFI MAUMBO.
Hili ni tawi la sarufi ambalo hujishughulisha na uchunguzi wa maumbo mbalimbali ya maneno katika lugha ya Kiswahili. Maumbo hayo ni; silabi, mofimu na neno lenyewe.

A.    Silabi
Silabi ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho kwacho sauti za
Lugha hutamkwa mara moja kwa pamoja kama fungu moja la sauti. Kuna aina mbili za silabi, yaani silabi fungenasilabi huru.
Silabi huruni zile ambazo huishia na irabu.
Kwa mfano; la, ma, kwa, mba, n.k.
 Ilhalisilabi fungeni zile zinazoishia na konsonanti ambapo katika lugha ya Kiswahili ni nadra kuzipata maana lugha hii inatumia silabi huru lakini hupatikana katika maneno ya Kiswahili yanayokopwa kutoka katika lugha nyingine.
            Kwa mfano;   Alhamisi – a-l-ha-mi-si
                                    Taksi     - ta-k-si
Miundo ya Silabi za Kiswahili
a.      Muundo wa irabu peke yake (I) - Yapo maneno katika lugha ya Kiswahili yanayoundwa na irabu peke yake kama silabi. Mfano; u+a = Ua, o+a = Oa, a+u = Au, n.k.
b.      Muundo wakonsonanti pekee (K) – Kiswahili hakina maneno mengi yanayoundwa na silabi pekee isipokuwa maneno machache ambayo huwa ni ya nazali /M/ na /N/ na huwa zinatumika ama mwanzoni au katikati ya neno. Mfano; m+ke = Mke, m+bwa =Mbwa, n+chi = Nchi n.k
c.       Muundo wa konsonanti na irabu (KI) – Katika muundo huu konsonanti hutangulia irabu. Mfano; b+a = Ba, k+a = Ka n.k.
d.      Muundo wa konsonanti mbili na irabu (KKI) – Katika muundo huukonsonanti mbili hutangulia irabu. Mara nyingi konsonanti ya pili huwa ni kiyeyusho. Mfano; k+w+a = Kwa, m+w+a = Mwa, b+w+a = bwa, n+d+e = Nde, n.k.
e.       Muundo wa konsonanti tatu na irabu (KKKI) – Muundo wa namna hii hujitokeza katika maneno machache. Mfano; Bambwa, Tingwa, Tindwa, Mbwa, n.k.
f.       Muundo wa silabi funge – Huu hujitokeza katika maneno machache ambayo huwa ya mkopo. Mfano; Il-ha-li = Ilhali, Lab-da = Labda
B.     Mofimu
Mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha lugha ambacho kina uwezo wa kusitiri maana ya neno ambalo kwalo limeundwa. AU ni kipashio kidogo kabisa cha lugha chenye maana kisarufi.

                                    AINA ZA MOFIMU
Mofimu huru ni aina ya mofimu ambayo huweza kusimama pekee na kujitosheleza kimaana yaani huwa na sifa ya neno. Mfano; mama, Baba, Dada, Kaka, Mjomba, Shangazi n.k. Kwa kuangalia utagundua kuwa mofimu huru haziwezi kugawanyika zaidi na kubeba maana kisarufi, kwa maana kwamba mofimu ‘baba’ ikigawanywa ba-ba, ‘ba’ hii haina maana yoyote kisarufi zaidi ya kuwa silabi.

Mofimu tegemezini aina ya mofimu ambayo huweza kuvunjwavunjwa na kubeba maana kisarufi, mofimu tegemezi hutegemeana ili kuleta maana kamili ya neno.
Mfano; neno ‘anakula’ limeundwa na mofimu zifuatazo:- [a-na-kul-a] ambazo kila moja hubeba dhana Fulani ya kisarufi.

VIAMBISHI
            Ni mofimu zinazopachikwa nyuma au mbele ya mzizi wa neno ili kubadilisha dhana ya neno. Kwa kuwa mofimu hizo hupachikwa sehemu mbili tofauti, tunapata aina mbili za viambishi kwa mujibu wa nafasi zake katika nenoyaani; viambishi awaliambavyo hupachikwa mwanzoni au nyuma ya mzizi wa neno,viambishi katiambavyo hupachikwa katikati ya neno (Kiswahili hakina viambishi hivi) na viambishi tamatiambavyo hivi hupachikwa mbele au mwishoni mwa mzizi wa neno.
Mfano:-
VIAMBISHI AWALI
MZIZI WA NENO
VIAMBISHI TAMATI
NENO JIPYA
    A
    na
           chez
     ew
    a
Anachezewa
    Wa
     li
           chez
     ean
    a
Walichezeana
    Tu
    ta
           chez
     e
    a
Tutachezea


1.      Viambishi awaliHivi hupachikwa kabla ya mzizi wa neno na huwa ni vya aina tisa:-
i.                    Viambisha awali vya nafsi- hivi hudokeza upatanishi wa  nafsi katika kitenzi, zipo nafsi tatu, nafsi ya kwanza, ya pili, nay a tatu.

NAFSI
UMOJA
UWINGI
Ya Kwanza
Ni-
Tu-
Ya Pili
U-
M-
Ya Tatu
A-
Wa-M


Mfano:-Ninalima
            Tunacheza

ii.                  Viambishi awali vya ngeli- hivi hupatikana mwanzoni mwa nomino au vivumishi ili kudokeza hali ya umoja na uwingi.

Mfano:-Mtu (umoja) – Watu (uwingi)
            Msafi (umoja) – Wasafi (uwingi)

iii.                Viambishi awali vya ukanushi - hivi hudokeza hali ya uhasi wa tendo. Huwakilishwa na mofimu (ha-) na (si-)

Mfano:- Amekula (uyakinifu) – Hajala (ukanushi), Nakula (uyakinifu) – Sili (ukanushi)
iv.                Viambishi awali vya Njeo- hivi hudokeza nyakati mbalimbali ambazo ni wakati uliopita, uliopo na ujao.

NYAKATI
MOFIMU
Uliopo
-Na-
Uliopita
-li-
Ujao
-Ta-

            Mfano:- Mlituona
                          Utakuja

v.                  Viambishi awali vya hali- hivi hudokeza hali mbili za nyakati ambazo ni mazoea ambayo huwakilishwa na mofimu {hu} na timilifu inayowakilishwa na mofimu {me}.
Mfano:-Hucheza
              Amelima

vi.                Viambishi awali vya masharti-hivi hudokeza hali ya masharti au uwezekano katika tendo. Mofimu hizo ni kama –ki-, nge-, ngali- n.k.

Mfano:- ukija
              Ungekuja
               Angalimkuta

vii.              Kiambishi cha urejeshi wa mtenda (kiima)- mhiki hudokeza urejeshi wa nomino inayotenda katika kitenzi.

Mfano: - Aliyekuja {-ye-} hudokeza urejeshi wa mtenda.

viii.            Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa au mtendewa (shamirisho) – hivi huwakilisha mtendwa au mtendewa wa jambo.
Mfano; Nilimpiga, Uliukata, Nimeipenda, Wameniteta.

ix.                Kiambishi awali cha kujirejea (kujitendea) – hiki huwakilishwa na mofimu (-ji-)
Mfano; kujipenda

2.      Viambishi tamati– Hivi hudokeza kauli mbalimbali za vitenzi.
Mfano: - Anacheza – kutenda
Unachezwa- Kutendwa
              Utachezewa- Kutendewa
               Nimemlia- Kutendea
              Wamewasomesha- Kutendesha n.k

Mzizi
Kiambishi cha Kauli
Kiambishi tamati maana
Neno jipya
Kauli
Viambishi vya kauli
Chez

a
Cheza
Kutenda
-a

e
a
Chezea
kutendea
-e-
Pig
ian
a
Pigiana
Kutendeana
-ian-/-ean-

iw
a
Pigiwa
Kutendewa
-iw-/ew-
Som
esh
a
Somesha
Kutendesha
-ish-/esh-

eshw
a
Someshwa
Kutendeshwa
-ishw-/eshw-
Lim
ik
a
Limika
Kutendeka
-ik-/-ek-

an
a
Limana
Kutendana
-an-

w
a
Limwa
Kutendwa
-w-

DHANA YA MZIZI NA SHINA LA KITENZI

Mzizi wakitenzini sehemu ya neno inayobakia mara baada ya kuondoa viambishi vyote vya awali na tamati katika neno hilo. Mfano: - a-na-chez-a {-chez-}, m-ku-lim-a {-lim-}
Mzizi fungeni ule ambao hauwezi kujikamilisha kimaana yaani hauwezi kusimama kama neno. Mfano; -lim-, -chez-, -imb- n.k.
Mzizi huruni ule ambao huweza kusimama kama neno na ukichanganuliwa zaidi hupoteza maana yake ya msingi. Mfano; Kinu, Kazi, Arifu, Sali n.k.


Shina la kitenzini sehemu ya neno ambayo huongezwa viambishi fuatishi (tamati) au nisehemu ya neno ambayo hubakia baada ya kuondolewa viambishi tangulizi. Mfano:- chez+a = cheza, lim+a = lima. Sehemu hii ya neno hutumika kuundia neno jipya.
Shina sahili – hili ni shina ambalo huundwa na mofimu moja tu ambayo ni mzizi wa neno hilo, huwa ni mofimu huru, Mfano; Kesho, jana, kitabu, jarida n.k.
Shina changamano – shina hili huundwa na mzizi na kiambishi tamati maana. Mfano; cheka, lala, lia, kula n.k
Shina ambatani – shina hili huundwa na mofimu mbili ambazo ni huru. Mfano; mwana + kwenda = mwanakwenda, mbwa + mwitu = mbwamwitu

           
UAMBISHAJI NA MNYUMBULIKO WA MANENO
Uambishaji
Uambishaji ni ule utaratibu wa kuongeza viambishi katika mzizi wa nenoili kulipa neno maana ya ziada. AU ni hali ya kubadilishabadilisha mofimu katika mzizi wa neno ili kuonesha upatanisho wa kisarufi katika tungo hiyo.
Kiambishi:
Kiambishi ni sehemu (mofu) ambayo huambikwa kwenye mzizi wa neno ili kulipa neno hilo maana ya ziada. Tunapopachika viambishi hivyo mwanzoni mwa mzizi wa neno hali hiyo huitwa ‘uambishaji’. Uambishaji upo wa aina mbili; Unyambuaji au unyambulishi: Huu ni aina ya uambishaji unaosababisha neno kubadilika kutoka kategoria moja hadi nyingine. NaMnyambuliko:Ni aina ya uambishaji ambao huhusisha kurefusha nenona kuliweka katika hali tofauti za katagoria ileile.
Uambishaji wa kategoria mbalimbali za maneno.
Uambishaji wa vitenzi – Uambishaji wa vitenzi hujitokeza kwa kutegemea dhima tofauti tofauti za mofimu kama vile:-
        i.            Viambishi vya nafsi
      ii.            Viambishi vya njeo
    iii.            Viambishi vya ukanushi
    iv.            Viambishi vya urejeshi
      v.            Viambishi vya hali
    vi.            Na viambishi vya kujitendea
Mfano; mzizi –lim- unaweza kupachikwa viambishi hivyo na kuweza kubadilika kidhana kama ifuatavyo:-
A-na-lim-a
Hu-lim-a
U-me-lim-a
Ni-na-vyo-lim-a n.k.

Uambishaji wa majina– Uambishaji wa majina huwa unazingatia upatanisho wa kisarufi kimofolojia ambao hujikita katika kuangalia alomofu tofauti zinazowakilisha ngeli moja katika umoja na uwingi wa majina hayo.  Kwa mfano:-
UMOJA
WINGI
ALOMOFU
m-tu
Wa-tu
M/WA
m-ti
mi-ti
M/MI
Ki-ti
vi-ti
KI/VI
u-gonjwa
Ma-gonjwa
U/MA
Ø-fisadi
Ma-fisadi
Ø/MA
Ø-kaka
Ø-kaka
Ø/ Ø

Uambishaji wa vielezi– Vielezi katika lugha ya Kiswahili havitokani na kategoria nyingine ya maneno, bali ni maneno ya kawaida yanayopatikana katika lugha na si rahisi kupachika mofimu yoyote katika maneno hayo isipokuwa vielezi vichache ambavyo hupatikana kwa kupachikwa kiambishi awali cha namna {ki-} katika kivumishi au nomino mfano: ki-jinga, ki-janja, ki-toto, ki-raia, ki-puuzi n.k.
UNYAMBULISHAJI
Ni hali ya kupachika viambishi tamati katika mzizi wa neno. Mofimu hizo huitwa mofimu fuatishi.
Unyambulishaji wa kategoria mbalimbali za maneno ya Kiswahili.
        i.            Viwakilishi. Mfano; Mimi = miye, Sisi = siye, Ambalo, Ambacho, Ambao,Ambaye n.k.
      ii.            Majina. Mfano: Nyumba+ni = Nyumbani, Shamba+ni = Shambani, n.k.
    iii.            Vivumishi. Mfano: Safi = Safisha, Refu = Refushan.k.
    iv.            Vitenzi. Mfano: Lima-limika-limishwa-limwa-limiana-limiwa n.k.
Ukitazama kwa makini utangundua kwamba unyambulishaji mara nyingi hubadilisha neno kutoka katika kategoria moja na kuipeleka katika kategoria nyingine.
DHIMA ZA UNYAMBULISHAJI
        i.            Kuongeza msamiati wa lugha ya Kiswahili.
      ii.            Kuzalisha kauli mbalimbali za vitenzi vya Kiswahili
    iii.            Hupanua maana ya neno.


  COMMENT BOX / SANDUKU LA MAONI